Polisi yaahidi kuendeleza ushirikiano na TAMESO T
24 June 2026, 14:26

Ushirikiano kati ya serikali, wataalamu wa afya na waganga wa tiba asilia unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa huku vitendo vinavyochochewa na imani potofu vikidhibitiwa kwa manufaa ya jamii.
Na Anwary Shaban.
Jeshi la Polisi nchini limeahidi kuendelea kushirikiana na Chama cha Waganga wa Tiba Asilia Tanzania (TAMESO T) katika kupambana na ramli chonganishi na imani potofu zinazochochea vitendo vya uhalifu katika jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Alex Mkama, amesema ushirikiano kati ya jeshi la polisi, wataalamu wa afya na waganga wa tiba asilia utasaidia kupunguza madhara yatokanayo na imani za kishirikina na kuimarisha usalama wa wananchi.
CP Mkama ameyasema hayo katika hafla ya mahafali ya wahitimu wa mafunzo ya tiba asilia iliyofanyika Kibaigwa, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, ambapo amewapongeza wahitimu hao kwa kukamilisha mafunzo yao kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kutoka serikalini.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Musa Lipukuta, amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania hutumia tiba asilia, hali inayoonesha umuhimu wa kuwafikia wananchi walipo kwa kuwapatia elimu sahihi ya afya na matumizi salama ya tiba asilia.
Naye Raymond Ngonyani, akisoma risala kwa mgeni rasmi, amesema kuwa Chama cha TAMESO T kimeazimia kuwa tarehe 26 Februari ya kila mwaka itumike kama siku maalum ya wanachama kukutana, kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili chama hicho.
Sanjari na hilo, Katibu Mkuu wa TAMESO T Taifa, Lucas Mlipu, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wake na kueleza dhamira ya chama hicho ya kupanua shughuli zake hadi Zanzibar ili kuimarisha mshikamano na kuongeza huduma kwa wananchi.