Dodoma FM

Wananchi Ilangali B walia uharibifu wa mto Kizogo

20 July 2026, 17:34

Mto huo umebeba maisha ya wananchi kwani hakuna huduma ya visima virefu vya maji ya bomba hivyo wengi hulazimika kutumia maji ya mtoni. Picha na Dodoma fm.

Licha ya wadau wa mazingira kufika eneo la uchimbaji kufanya tathmini na kutoa maelekezo lakini kumekuwa hakuna utekelezaji wowote.

Na Anwary Shaban.

Wakazi wa kitongoji cha Ilangali “B” Kata ya Manda Wilaya ya Chamwino wameendelea kulia na uharibifu wa chanzo cha maji katika mto kizogo ambao ndio unatumika Kwa asilimia kubwa kuhudumia wakazi hao na kitongoji jirani cha mafulungu.

Wakizungumza na taswira ya habari wananchi hao wamesema mto huo umebeba maisha ya wananchi kwani hakuna huduma ya visima virefu vya maji ya bomba hivyo wengi hulazimika kutumia maji ya mtoni.

Wananchi hao wamesema licha ya maji yam to huo kuwa tegemeo la kijiji chao lakini kwasasa maji ya mto huo yanaathiriwa na maji taka yanayo tiririka kutoka katika machimbo ya dhahabu ya kitongoji cha Mafulungu hali inayo hatarisha afya za wananchi .

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilangali Bw. Anania Ngodingo anasema tatizo hili wamesha liliripoti mara kwa mara katika mamlaka husika lakini hakuna suluhisho lolote hivyo wananiomba serikali kuwachimbia visima ili kuepukana na athari itakayo tokana na maji hayo kuharibiwa.

Aidha Ngodingo Ameongeza kuwa licha ya wadau wa mazingira kufika eneo la uchimbaji kufanya tathmini na kutoa maelekezo lakini kumekuwa hakuna utekelezaji wowote

Kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha sita (6) inasema mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira.