Wakulima watakiwa kutumia vema mvua za El nino kwa mbinu bora za kilimo
1 September 2026, 16:44

Wananchi wameendelea kusisitiza umuhimu wa kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mwenendo wa mvua, huku wakitakiwa kuchukua tahadhari mapema kwa kusafisha mifereji, na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.
Na Peter Katemi.
Wakulima wametakiwa kujiandaa kukabiliana na mvua za El nino zinazo tarajia kuanza kunyesha pamoja na kuzingatia kanuni za kilimo ili maji yasiathiri mashamba yao.
Hivi karibuni mamlaka ya hali ya hewa (TMA) ilimetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Desemba) 2026, ikitoa angalizo la msimu huo kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa iliyotokana na joto la bahari kuwa Juu ya Wastani
Je, wananchi na wakulima wamejiandaa vipi kukabiliana na mvua hizo ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza?
Taswira ya habari imezungumza na Bw. Henry Charles ambae ni Afisa kilimo yeye anasema shughuli za kilimo zinaweza kuendelea kama kawaida licha ya uwepo wa mvua za El Niño, lakini wakulima wanapaswa kutumia fursa ya mvua hizo kwa wakati na kujiandaa mapema kwa kuhakikisha wanatengeneza mifereji katika mashamba yao ili kuzuia maji kutuama na kusababisha uharibifu wa mazao.
Aidha, amewataka wananchi na wakulima kufuata ushauri unaotolewa na maafisa ugani kuhusu namna bora ya kujiandaa na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Nao baadhi ya wananchi wameipongeza mamlaka ya hali ya hewa kwa kutoa taarifa na tahadhari mapema, huku wakiiomba Serikali na wataalamu kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kujiandaa, maeneo ya kuepuka na hatua za kuchukua ili kulinda maisha na mali zao dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza dhidi ya mvua hizo.