Maafisa usafirishaji watakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani
11 August 2026, 17:44

Jeshi la polisi limeendelea kuwataka madereva wa bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kutumia vifaa vya kinga ili kujilinda wenyewe, pamoja na watumiaji wengine wa barabara.
Na Ramadhani Juma.
Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani linawataka madereva wa bodaboda kuzingatia sheria za barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu, kudhibiti mwendo na kuepuka kubeba abiria zaidi ya mmoja ili kupunguza ajali za barabarani.
Taswira ya habari imezungumza na mmoja wa askari wa usalama barabarani katika eneo la Mipango ambapo amesema, baadhi ya makosa yanayofanywa na madereva wa bodaboda ni pamoja na kutokuvaa kofia ngumu, kutokuzingatia sheria za barabarani na kuendesha kwa mwendo wa kasi.
Amesema jeshi la polisi huchukua hatua dhidi ya madereva bodaboda wanaokiuka sheria, ikiwemo kuwatoza faini na kuwapeleka mahakamani kulingana na kosa walilolifanya. Huku wakiendelea kuwapatia madereva elimu ya kutosha kuhusu sheria na usalama barabarani.
Taswira ya habari imewatafuta baadhi ya madereva wa bodaboda wao wamesema, wakati mwingine hulazimika kutokuzingatia baadhi ya sheria kutokana na shinikizo la abiria wanaotaka kuwasili haraka, huku mwendo wa kasi ukiwasaidia kufanya safari nyingi na haraka.