Mama lishe Machinga walalamikiwa kumwaga maji taka mitaroni
11 August 2026, 17:20

Changamoto ya miundombinu ya soko nayo inachangia tatizo hilo, huku jitihada za kutatua kero hiyo bado zinaendelea.
Na Grace Bugodi.
Wafanyabiashara wa soko la Machinga jijini Dodoma wamelalamikia tabia ya baadhi ya mama lishe kumwaga maji taka katika mitaro ya eneo la soko hali inayo pelekea harufu mbaya katika eneo hilo.
Wakiongea na Taswira ya Habari, baadhi ya wafanyabiashara wamesema harufu hiyo husababishwa na baadhi ya mama lishe pamoja na wafanyabiashara wanaomwaga maji machafu kwenye mitaro, huku wengine wakidai uongozi wa soko hauchukui hatua za kutosha kuhakikisha usafi unaimarika.
Akizungumzia malalamiko hayo makamu mwenyekiti wa Soko la Machinga Bw. Shaban Seleman amesema uongozi una utaratibu wa kufanya usafi kupitia wafanyakazi wake, lakini baadhi ya wafanyabiashara hukusanya maji machafu na kuyamwaga kwenye mitaro nyakati za jioni jambo linalochangia harufu hiyo.
Ameongeza kuwa changamoto ya miundombinu ya soko nayo inachangia tatizo hilo, huku jitihada za kutatua kero hiyo bado zinaendelea.