Dodoma FM

INEC: Asasi za kiraia zenye kibali zitoe elimu ya mpiga kura

9 September 2025, 1:30 pm

Picha ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani, wakati wa kufungua kikao kazi kati ya Tume na taasisi pamoja na asasi hizo.Picha na Tume ya uchaguzi.

Amesisitiza kuwa taasisi na asasi hizo haziruhusiwi kuwapa watu wengine, taasisi au asasi vibali walivyopewa, na kwamba vibali hivyo vinapaswa kutumiwa na walengwa pekee.

Na Yussuph Hassan.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imezitaka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na weledi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani, ametoa wito huo Septemba 8, 2025, wakati wa kufungua kikao kazi kati ya Tume na taasisi pamoja na asasi hizo kilichofanyika mkoani Dodoma.

Kailima ameongeza kuwa INEC inatarajia kuona taasisi na asasi za kiraia zikitoa elimu iliyolengwa, huku zikisisitiza masuala yanayowapa wananchi, wagombea, na vyama vya siasa uelewa juu ya kushiriki katika kampeni kwa amani na utulivu, ikiwa ni pamoja na kuelewa vyema utaratibu wa kupiga kura.

Kikao kazi hicho kimewahusisha viongozi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wawakilishi wa taasisi na asasi 164 zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa.