Dodoma FM

Afariki Dunia baada ya kukanyagwa na Tembo

23 April 2025, 6:13 pm

Picha ni baadhi ya waombolezaji wakiwa katika msiba huo katika kijiji cha Chifutuka.Picha na Yussuph Hassan.

Ikumbukwe kuwa hili ni tukio la Nne la Mwananchi kuuliwa na tembo katika kata ya Chifutuka ambapo Tembo wamekuwa wakitoroka katika hifadhi za kuingia katika makazi ya wananchi licha ya Askari wa TAWA kufanya jitihada za kuwafukuza katika maeneo ya wananchi lakini bado changamoto inaendelea.

Mkazi mmoja aliyefahamika kwa jina la Hosea Mtubwa amefariki dunia baada ya kukanyangwa na tembo katika kijiji cha Chifutuka Wilayani Bahi mkoani Dodoma.

Akithibitisha kutokea kwa Tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho Julias Chilingo amesema tarehe 21 mwezi wa nne mwaka huu majira ya saa kumi na mbili na nusu Alfajiri alipokea taarifa juu ya mkazi wake Hosea Mtibwa kukutwa amefarikia dunia.

Gerrad Jeremia Mtubwa ni kaka wa Marehemu anasema ndugu yake alisherehekea vyema sikukuu ya Pasaka lakini siku ya pili ya Jumatatu akiwa ametoka matembezi katika eneo la katikati ya kijiji hicho ndipo alikutana na tembo na kuuwawa.

Picha ni Mwenyekiti wa kijiji hicho Julias Chilingo akiongea wakati wa mazishi ya mwananchi huyo.Picha na Yussuph Hassan

Kutokana na Tukio hilo Mbunge wa Jimbo la Bahi Mhe Keneth Nollo alifanikiwa kufika katika Msiba wa Mkazi huyo na kutoa pole kwa wafiwa na kuahidi kufanya juhudi za kukutana na Waziri wa Malisili na utalii ili kujua hatma ya kumaliza changamoto ya tembo kuvamia makazi ya watu na kuharibu mazao yao.

Aidha Mamlaka ya Wanyama Pori nchini TAWA wameendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wa Vijiji hivyo vilivyo hatarini na wanyama wakali na waharibifu kuchukua angalizo kwa kuacha kuvaa mavazi yenye rangi zenye mng’ao mfano Rangi nyekundu,Njano na Nyeupe na kuacha tabia ya kutembea usiku.

Habari kamili