Mama lishe 300 wapatiwa mafunzo ili kukua kiuchumi
20 May 2026, 11:12

Kwa Dodoma, wajasiriamali 300 watakaoshiriki programu hii watapatiwa kila mmoja jiko banifu kama sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Na Mariam Kasawa.
Jumla ya mama Lishe 300 wamepatiwa mafunzo ya Rise mama lishe yaliyoandaliwa na Benki ya Stanbic kwa Lengo la kumsaidia mama lishe kukua kiuchumi.
Benki ya Stanbic imetoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Sido, bakhresa group pamoja na GIZ ambalo wajasiriamali 300 wa biashara za chakula wamepatiwa mafunzo ya vitendo pamoja na majiko banifu yatakayowasaidia kupunguza gharama, kuboresha usalama na kuimarisha biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo Jijini Dodoma, meneja wa Benki ya Stanbic Tawi la Dodoma Joan Mbise amesema zaidi ya mama Lishe elfu tatu wameshiriki ktk program hii ya Rise mama lishe ndani ya miaka mitatu iliyopita.
Mkurugenzi wa mafunzo na Tawala za Mikoa Sido, CPA George Kasinga amesema kwa miaka mingi Sido imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kukuza na kuendeleza biashara ndogondogo na za kati kupitia mafunzo ya ujasiriamali, ushauri wa biashara, ubunifu pamoja na huduma za maendeleo ya biashara huku akieleza maeneo yaliyoguswa kwenye mafunzo hayo.

Naye Bi Lisa kutoka GIZ amesema haya si mafunzo tu Bali ni uwekezaji kwa wanawake wa kitanzania.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza namna watakaenda kufanya biashara zao kutokana na Elimu waliyopata Ili kuendelea kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kupitia awamu ya mwaka 2025 hadi 2026, Stanbic Bank na GIZ wanalenga kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali wapatao 2,000 kwa kuwapatia elimu ya biashara, stadi za usimamizi wa fedha, uelewa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na vifaa vinavyogusa mahitaji halisi ya biashara zao za kila siku.