Dodoma FM

Serikali yaombwa kushughulikia chanzo cha changamoto za vijana mpwapwa

7 August 2026, 11:03

Ukosefu wa ajira na msongo wa mawazo ni miongoni mwa changamoto zinazo wakumba vijana. Picha na Stephen Noel

Vijana wanapaswa kuzingatia maadili, kufanya kazi kwa bidii, kutumia fursa zilizopo na kukabiliana na changamoto kwa njia halali ili kujijengea maisha bora na kuchangia maendeleo ya jamii
.

Na Stephen Noel.

Vijana wa vyuo vya kati wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuweka mkazo katika kushughulikia vyanzo vya changamoto zinazowakabili vijana badala ya kujikita katika kushughulikia matokeo yake pekee.
Ombi hilo limetolewa na baadhi ya vijana hao walipozungumza na Dodoma FM katika mahojiano maalumu, ambapo walieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya, ukosefu wa ajira na msongo wa mawazo ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri maisha na maendeleo ya vijana wengi.

Wamesema changamoto hizo zinachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, migogoro ya kifamilia na wazazi, pamoja na msongo wa mawazo unaowafanya baadhi ya vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vinavyohatarisha mustakabali wao.

Kwa mujibu wa vijana hao, hatua madhubuti za kuimarisha ajira, huduma za ushauri nasaha na malezi bora ya familia zinaweza kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayowakabili vijana.
Wamesisitiza kuwa kushughulikia chanzo cha changamoto hizo kutasaidia kujenga kizazi chenye afya njema ya akili, maadili mema na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto hizo na inaendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kuwawezesha vijana. Amewataka vijana kuepuka kuiga maisha yanayoonekana kwenye mitandao ya kijamii ambayo wakati mwingine hayalingani na uhalisia.