Ukosefu wa elimu ya ardhi wachangia migogoro vijijini
10 September 2026, 16:47

Wananchi wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu upimaji na urasimishaji wa ardhi, ili kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kwa njia halali na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka sahihi za umiliki.
Na Victor Chigwada.
Kukosekana kwa ufanisi katika upimaji na urasimishaji wa ardhi pamoja na ukosefu wa elimu kwa wananchi kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia migogoro ya ardhi katika maeneo ya vijijini.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Chamwino, ambao ni miongoni mwa walioathirika na migogoro ya ardhi katika maeneo yao, wamesema changamoto hiyo inachangiwa pia na uwepo wa kampuni nyingi za upimaji ardhi, huku baadhi yao zikifika katika maeneo hayo bila taarifa maalumu.
Wamesema mwingiliano kati ya kampuni binafsi za upimaji ardhi na zile za Serikali umechangia baadhi ya wananchi kuingia katika migogoro ya umiliki wa ardhi.
Aidha, wameeleza kuwa ukosefu wa elimu kuhusu taratibu za umiliki na urasimishaji wa ardhi nao ni changamoto inayochangia kuibuka kwa migogoro hiyo.