Ujenzi wa uwanja wa msalato Dodoma wafikia asilimia 89
25 September 2026, 16:23

Na Mwandishi wetu.
TANROADS imewaelekeza mameneja wa mikoa kujiandaa kukabiliana na athari za mvua kubwa zinazotarajiwa Oktoba hadi Desemba, huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari wanapotumia barabara na vivuko wakati wa mvua.
Ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Dodoma, umefikia asilimia 89, huku hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za usalama na ithibati ya anga zikiendelea.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema miundombinu ya uwanja huo inatarajiwa kukamilika Desemba 27, 2026, wakati majengo yakitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026.
Amesema ujenzi wa majengo muhimu, ikiwemo jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, kituo cha zimamoto, kituo cha umeme na kituo cha huduma za hali ya hewa, umefikia asilimia 79.
Besta amesema kuanza kwa safari za ndege kutategemea kukamilika kwa mchakato wa certification pamoja na kuchapishwa kwa taarifa rasmi za matumizi ya uwanja huo katika mifumo ya kimataifa ya usafiri wa anga.
Uwanja wa Msalato umejengwa kwa kiwango cha 4E cha ICAO, kinachowezesha kuhudumia ndege kubwa na safari za ndani na kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika usafirishaji wa abiria na mizigo.