Wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakiwa kuhamasisha uchunguzi wa macho
24 November 2026, 16:22

Wananchi wanapaswa kuachana na tabia ya kusubiri hadi matatizo ya macho yanapokuwa makubwa ndipo watafute huduma za afya, badala yake wawe na utaratibu wa kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara.
Na Stephen Noel.
Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wilayani Mpwapwa wametakiwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya ya macho mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa yanayoweza kusababisha upofu na upotevu wa uwezo wa kuona.
Wito huo umetolewa na Afisa Miradi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Sightsavers, Bi. Magdalena Focas, wakati akizungumza na wahudumu hao katika semina ya siku mbili inayolenga kuwajengea uwezo wa kutambua dalili za awali za magonjwa ya macho.
Bi. Focas amesema kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhusu magonjwa ya macho kutasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi na kuwahamasisha kutafuta huduma za uchunguzi na matibabu kwa wakati, hatua itakayosaidia kupunguza hatari ya upofu unaoweza kuzuilika.
Kwa upande wake, Daktari wa Magonjwa ya Macho katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Asern Ngowi, amesema upofu unaweza kuongeza utegemezi wa mtu kwa familia na jamii, hivyo ni muhimu wananchi kuzingatia uchunguzi wa afya ya macho ili kubaini na kutibu magonjwa mapema.