Dodoma FM

Watumiaji wa bima nchini waongezeka kufikia milioni 26.6

20 October 2026, 16:31

Picha ni Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, akijadili kuhusu bima na wadau siku ya uzuinduzi. Picha na Anwary Shabani.

Ongezeko la watumiaji wa bima linaendelea kuweka msisitizo katika umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu bidhaa na huduma za bima, ili wananchi wengi zaidi waweze kuzitumia kama njia ya kujikinga na majanga na kuimarisha usalama wao wa kifedha.

Na Anwary Shabani.

Idadi ya watumiaji wa bidhaa na huduma za bima nchini imeongezeka kutoka watu milioni 5.6 mwaka 2021 hadi milioni 26.6 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko linaloashiria kuimarika kwa uelewa na imani ya wananchi kuhusu umuhimu wa bima katika kukabiliana na vihatarishi mbalimbali.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa soko la bima Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha sekta ya bima inakuwa imara, himilivu na endelevu, kwa manufaa ya watumiaji na wawekezaji.

Aidha, Dkt. Saqware amesema soko la bima nchini lina uwezo wa kuhimili vihatarishi vya kiuchumi kwa kiwango kinacholingana na asilimia 94.5 ya pato la taifa, hali inayoonesha mchango na uwezo wa sekta hiyo katika kutoa kinga dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uchumi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa mtaa wa Miyuji jijini Dodoma wameeleza umuhimu wa kuwa na bima, wakibainisha kuwa wananchi wengi hukumbana na changamoto za kifedha pale wanapokumbwa na majanga bila kuwa na kinga ya bima.

Simulizi na Anwary Shabani.