Dodoma FM

DUWASA yasogeza huduma ya maji karibu na wananchi

6 October 2026, 11:23

Picha ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa DUWASA, Lena Mwakisale, kutembelea mabanda ya huduma kwa wateja katika maeneo ya Nkuhungu. Picha na Anwary Shabani.

DUWASA imewasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, ikiwa ni hatua ya kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupokea maoni na kutatua changamoto zinazohusu maji na usafi wa mazingira jijini Dodoma.

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeeleza kuwa imejipanga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kupokea na kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa DUWASA Dodoma, Lena Mwakisale, wakati alipotembelea mabanda ya huduma kwa wateja yaliyopo maeneo ya Nkuhungu, Msalato na Nzuguni jijini Dodoma.

Mwakisale amesema DUWASA imeamua kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi, kupunguza umbali wa kufika katika ofisi za mamlaka hiyo, pamoja na kutoa fursa ya wananchi kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja.

Aidha, Mwakisale amewataka wananchi kutumia fursa ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kufika katika mabanda ya DUWASA yaliyopo maeneo mbalimbali jijini Dodoma, akieleza kuwa wiki hiyo ni muhimu kwa wananchi kupata huduma, kutoa maoni na kueleza changamoto zinazohusu huduma za maji na usafi wa mazingira.

Amesema DUWASA inatambua na kuthamini mchango wa wananchi katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya jiji la Dodoma.

Simulizi na Anwary Shabani