Wazalishaji wa chumvi na chokaa Nzuguni waomba mikopo na vifaa vya kisasa
27 November 2026, 17:09

Wazalishaji wa madini ya chumvi na chokaa katika Mtaa wa Chitelela, Kata ya Nzuguni jijini Dodoma, wameiomba Serikali kuwawezesha kupata mitaji, mikopo na vifaa vya kisasa vitakavyoboresha shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini hayo, ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wao.
Na Victor Chigwada.
Wamesema matumizi ya vifaa vya asili katika shughuli za uchimbaji na uzalishaji yamekuwa yakikwamisha maendeleo ya shughuli hiyo, hivyo kupata vifaa vya kisasa kutawawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa na kupanua soko la chumvi na chokaa wanachozalisha.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Ndg. Steven Masine, amesema shughuli za uzalishaji wa chumvi na chokaa zimekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa baadhi ya wakazi wa Chitelela, huku zikisaidia familia kujikimu na kugharamia mahitaji mbalimbali, ikiwemo elimu ya watoto wao.
Masine amesema iwapo wazalishaji hao watapata mitaji na vifaa vya kisasa, wataweza kuongeza uzalishaji na kukuza kipato chao zaidi, huku akieleza kuwa juhudi za awali za kuunda kikundi ili kupata mikopo ya Halmashauri hazikufanikiwa, hali iliyowakwamisha kupata fursa ya kuboresha shughuli zao za uzalishaji.