Wananchi Itiso walalamikia upungufu wa maji safi na salama
26 November 2026, 16:19

Wananchi wa Kijiji cha Itiso, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wamelalamikia ukosefu wa maji safi na salama, hali inayowalazimu kutumia maji ya korongo kwa matumizi ya nyumbani na mifugo, huku wakichangia gharama za upatikanaji wa maji hayo.
Na Victor Chigwada.
Huduma ya uhakika ya maji umekuwa ukiwaweka katika hatari ya kupata magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama, huku baadhi yao wakilazimika kutafuta maji nyakati za usiku kutokana na uhaba wa maji katika kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Bw. Halifa Punta, amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji, akieleza kuwa wananchi wamekuwa wakichimba visima vifupi katika korongo ili kupata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kila siku.
Punta amesema matumizi ya maji hayo yanaongeza hatari ya magonjwa, hasa wakati wa msimu wa mvua, ambapo maji yanayotiririka kutoka maeneo mbalimbali hubeba uchafu na kuingia katika vyanzo vinavyotumiwa na wananchi. Ameiomba Serikali kukamilisha mradi wa kisima cha maji kijijini hapo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.