Umuhimu wa matumizi ya takwimu rasmi katika kupanga maendeleo
17 November 2026, 15:54

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi sahihi ya takwimu rasmi, huku wananchi wakihimizwa kuthamini na kutumia takwimu katika kufanya maamuzi yatakayochochea maendeleo endelevu nchini.
Na Maiam Kasawa.
Matumizi ya takwimu rasmi yameelezwa kuwa msingi muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, miundombinu na ugawaji wa rasilimali za Serikali kulingana na mahitaji halisi ya wananchi.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Uratibu na Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Magreth Maganda, wakati akizungumza na kipindi cha Taswira ya Habari cha Dodoma FM kuelekea maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, yatakayotumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa takwimu na matumizi yake katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Magreth amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kuelimisha jamii kuhusu nafasi ya takwimu katika maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa na kutumia takwimu rasmi katika kufanya maamuzi mbalimbali.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, Magreth amesema yanalenga kuimarisha mifumo rasmi ya takwimu za maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi barani Afrika, jambo linaloendana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.
Aidha, amesema takwimu zinazokusanywa na kuchambuliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zina mchango mkubwa katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango yake kwa kuzingatia uhalisia wa mahitaji ya wananchi, ikiwemo kubaini maeneo yanayohitaji shule, hospitali na miundombinu mingine pamoja na kupanga ugawaji wa bajeti.