Dodoma FM

Utandawazi watajwa kuchangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto

16 October 2026, 16:59

Picha ni watoto wakiwa wanatumia matumizi ya simu katika mitandao ya kijamii kwa muda mrefu. Picha na Mwananchi.

Mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana unazidi kuibua wasiwasi katika jamii, huku matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii na udhaifu katika malezi vikitajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo, hali inayochochea wito wa wazazi na jamii kuimarisha usimamizi wa watoto na kurejesha misingi bora ya maadili.

Na Daniel Njau.

Matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yametajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto, vijana na jamii kwa ujumla, huku wazazi wakihimizwa kuimarisha malezi na kusimamia misingi bora ya maadili ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

Baadhi ya wananchi waliozungumza kuhusu suala hilo wamesema mmomonyoko wa maadili unachangiwa na malezi yasiyozingatia misingi bora ya nidhamu nyumbani na katika jamii inayowazunguka watoto, pamoja na baadhi ya wazazi kukosa uelewa wa kutosha kuhusu namna bora ya kuwalea watoto wao.

Kwa upande wake, Dastan Haule, mshauri wa malezi na familia, amesema baadhi ya wazazi wanachangia hali hiyo, huku maendeleo ya utandawazi yakiongeza changamoto katika malezi. Amesisitiza kuwa wazazi wana nafasi muhimu ya kuzuia mmomonyoko wa maadili kwa kuwajengea watoto nidhamu, kuwaongoza na kutimiza wajibu wao katika malezi.

Hivyo, jamii imetakiwa kushirikiana katika kutoa malezi bora, kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii na kukemea vitendo vinavyokiuka maadili, ili kujenga kizazi chenye nidhamu, uwajibikaji na misingi bora ya maadili ya Kitanzania.

Simulizi na Daniel Njau.