Idara ya mifugo yatakiwa kuongeza kasi ya chanjo ya wanyama Mpwapwa
28 September 2026, 16:46

Ushirikiano kati ya wananchi, wataalamu wa afya ya binadamu na mifugo ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Na Stephen Noel.
Serikali Wilaya ya Mpwapwa imetaka Idara ya Mifugo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu chanjo na utunzaji sahihi wa wanyama, hususan mbwa wanaoishi kwa ukaribu na binadamu, ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa na madhara yake.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Sophia Mfaume Kizigo, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Obert Mwalyego, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ilolo, mjini Mpwapwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mwalyego amesema utoaji wa elimu kwa jamii ni hatua muhimu katika kuzuia ugonjwa huo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwajibika katika malezi na utunzaji wa wanyama wao.
Amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha wanyama wanapatiwa chanjo na matibabu kwa wakati, pamoja na kuchukua tahadhari zinazohitajika ili kupunguza uwezekano wa madhara kwa binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Emanuel Lyimo, amesema maadhimisho hayo yametumika kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana ya Afya Moja (One Health), ambayo inasisitiza uhusiano kati ya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Dkt. Lyimo amesema jamii pia imepewa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.