Dodoma FM

Ubomoaji wa majengo maili mbili wapisha upanuzi wa barabara ya msalato

11 November 2026, 16:25

Picha ni zoezi la ubomoji likiendelea maeneo ya maili mbili jijini dodoma kupisha ujenzi wa barabara. Picha na Anwary Shabani.

Wakati baadhi ya wakazi wa eneo la Maili Mbili wakikabiliwa na huzuni kufuatia kubomolewa kwa nyumba na majengo yao, baadhi ya vijana wanaojishughulisha na biashara ya bodaboda wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa upanuzi wa barabara hiyo utakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya eneo hilo.

Na Anwary Shabani.

Hatua za kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma zimechukua sura mpya baada ya kuanza kwa ubomoaji wa nyumba na majengo katika eneo la Maili Mbili, Kata ya Kiwanja cha Ndege, hatua inayolenga kupisha ujenzi wa barabara ya njia nne itakayorahisisha  usafiri  kuelekea  Uwanja  wa  Ndege  wa  Kimataifa  wa Msalato.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, amesema ubomoaji huo unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika maeneo yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara ili kutoa nafasi ya utekelezaji wa mradi huo wa upanuzi.

Shekimweri amesema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, wananchi waliokuwa wakiishi au kufanya shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyoathiriwa walipatiwa taarifa mapema ili kujiandaa kuondoka, huku wale waliostahili kulipwa fidia wakiwa tayari wamepatiwa stahiki zao.

Ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuboresha muunganiko wa usafiri kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, huku utekelezaji wake ukiendelea kuhitaji ushirikiano kati ya mamlaka husika na wananchi.

Simulizi na Anwary Shabani.