Dodoma FM

Wakazi wa Mlowa barabarani walilia jengo la mama na mtoto

21 September 2026, 17:26

Picha ni mfano wa jengo la hospitali katika huduma ya mama na mtoto. Picha na Fulushangwe blog.

Wakazi wa vitongoji vya Mahuma na Mlowa B, Kata ya Mlowa Barabarani, Wilaya ya Chamwino, wameiomba Serikali kujenga jengo maalumu la mama na mtoto katika kituo cha afya cha kata hiyo, wakisema ongezeko la wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali limeongeza msongamano, hususani katika huduma za uzazi, licha ya kituo hicho kuwasaidia wananchi kupata huduma karibu na makazi yao.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa vitongoji vya Mahuma na Mlowa B, Kata ya Mlowa Barabarani, Wilaya ya Chamwino, wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo, huku wakiomba ujenzi wa jengo maalumu la mama na mtoto ili kupunguza msongamano wa wajawazito wanaofika kupata huduma.

Wamesema uwepo wa kituo hicho umesaidia kupunguza safari za kina mama wanaohitaji huduma za kujifungua, ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika vituo vingine vya afya.

Hata hivyo, wameeleza kuwa changamoto iliyopo ni uhaba wa nafasi kwa wajawazito wanaosubiri kupata huduma au kujifungua, hali inayosababisha kubanana katika eneo la huduma za uzazi.

Diwani wa Kata ya Mlowa Barabarani, Anjero Lukasi, amesema kituo hicho kinahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya za Bahi, Kongwa na Mpwapwa pamoja na Chamwino, jambo linalochangia kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za uzazi.

Amesema ombi la ujenzi wa jengo hilo tayari limewasilishwa serikalini, huku akieleza kuwa baadhi ya huduma ambazo hazikuwepo awali sasa zimeanzishwa na zinaendelea kutolewa kwa wananchi.

Simulizi na Victor Chigwada.