Wananchi watakiwa kuacha dhana potofu juu ya kuandika wosia
16 July 2026, 13:19

Jamii imehimizwa kufuata sheria na taratibu za mirathi pamoja na kuandika wosia mapema ili kulinda haki za warithi, kuimarisha amani ya familia na kuondoa migogoro inayoweza kuepukika.
Na Anwary Shaban.
Migogoro ya mirathi imeendelea kuwa chanzo cha migawanyiko katika familia nyingi nchini, hali inayochangiwa na kutokuwepo kwa wosia pamoja na uelewa mdogo wa sheria zinazohusiana na mirathi.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimewahimiza wananchi kuandika wosia mapema ili kulinda haki za warithi na kudumisha amani ndani ya familia.
Hayo yameelezwa na mwanasheria kutoka TAWLA,Bi Grace Mbenje, ambapo amesema kuwa mirathi ipo ya aina mbili; ile yenye wosia na ile isiyo na wosia, na kwamba kila aina ina taratibu zake za kisheria zinazopaswa kufuatwa pale changamoto zinapojitokeza.
Amefafanua kuwa mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 anaruhusiwa kisheria kuandika wosia, akisisitiza kuwa si lazima mtu awe na mali nyingi ndipo aandike wosia, bali ni hatua muhimu ya kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza baada ya kifo.
Akizungumzia changamoto zinazojitokeza katika masuala ya mirathi, Grace amesema mara nyingi mwanaume anapofariki dunia baadhi ya familia hushindwa kumwamini mjane kusimamia mali za marehemu, jambo ambalo huzua migogoro na kuvuruga mshikamano wa familia.
Aidha, ameitaka jamii kuacha tamaa ya mali za marehemu na kuzingatia maadili pamoja na utu, akieleza kuwa mtu anayeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hana umiliki wa mali hizo bali anapaswa kuzisimamia kwa mujibu wa sheria kwa manufaa ya warithi halali.
Nao baadhi ya wananchi wameeleza kuwa mitazamo hasi iliyopo kwenye jamii nyingi inapelekea watu kuamini kuwa kuandika wosia ni kujitabiria kifo hivyo watu wengi wanashindwa kufanya hivyo .