Dodoma FM

Serikali yawajengea bweni wanafunzi wa kike  wenye ulemavu Bahi

23 March 2022, 2:19 pm

Na; Mariam Matundu.

Wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika shule ya msingi Bahi sokoni wameishukuru serikali kwa kujengewa bweni  la wasichana shuleni hapo kwani hatua hiyo itaongeza ari kwa wazazi ya kuwapeleka watoto shule.

Baadhi ya wanafunzi hao wamesema iwapo bweni hilo litaanza kufanya kazi itasaidia wao kupata muda mwingi wa kujisomea kwa uangalizi wa walimu watakaokuwa wanaishi nao hapo .

Mwalimu Mustafa Ally ni mwalimu wa wanafunzi wenyeulemavu shuleni hapo amesema bweni hilo litasaidia kwa wanafunzi kujifunza kwa muda wa ziada kwa kuwa wapo watoto wenyechangamoto kubwa na kusababisha ujifunzaji wao kuwa wa taratibu .

Taswira ya habari imezungumza na baadhi ya wazazi ambapo licha ya kupongeza jitihada hizo wameiomba serikali kuwajengea bweni kwa ajili ya wanafunzi wavulana wenye ulemavu shuleni hapo.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Josephat Laulent amesema bweni hilo linatarajiwa kukamilika mwezi wa nne mwaka huu na pia ameiomba serikali kuifanya shule hiyo kuboreshwa na kupokea watoto wenye ulemavu kutoka maeneo tofautitofauti.

Shule ya bahi sokoni ni shule inayotoa elimu jumuishi ikiwa na jumla ya wanafunzi wenye ulemavu kumi na tisa wavulana 12 na wasichana 7 .