Dodoma FM

Chongolo: Watoto wasimamiwe waende shule

21 June 2023, 3:16 pm

Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo akiongea na wajumbe wa CCM baada ya kupatiwa historia fupi ya kambi ya wapigania uhuru wa nchi za Afrika iliyopo wilayani Kongwa. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Chongolo amesema wakati watoto wanapokuwa mashuleni sio wakati wa viongozi kukaa ofisini badala yake wajipange na kuratibu kuhakikisha watoto wote wanajiunga na masomo na si vinginevyo.

Na Bernadetha Mwakilabi.

Katibu mkuu wa Chama Chama Mapinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo amewataka watendaji wa vijiji na kata, wakurugenzi na wakuu wa idara kuhakikisha wanawasimamia watoto wote wanaotakiwa kwenda shule wanasoma.

Chongolo alimesema hayo alipotembelea wilayani Kongwa kwa ajili ya kuongea na wananchi na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Rais wa awamu ya sita Daktari Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

Chongolo amesema wakati watoto wanapokuwa shuleni sio wakati wa viongozi kukaa ofisini badala yake wajipange na kuratibu kuhakikisha watoto wote wanajiunga na masomo na si vinginevyo.

Aidha katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Bi. Sophia Mjema amewaeleza wananchi kuwa lengo la Mheshimiwa Rais kutaka watoto wasome masomo ya sayansi ni taifa kuwa na madaktari na wahandisi wetu wenyewe.

Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kongwa Mheshimiwa White Zuberi, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM ndugu Daniel Chongolo, na Mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel wakiwa katika ziara kukagua majengo yaliyotumika na wapigania uhuru yaliyopo katika shule ya sekondari Kongwa. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Katika ziara hiyo katika Kata ya Mtanana wananchi waliomba kupatiwa Kisima kipya cha maji kwani Kisima kilichopo kwa sasa kina changamoto suala ambalo Chongolo ameahidi kulifanyia kazi kwani maji ni uhai.

Akitolea ufafanuzi suala hilo Mkuu wa mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule aliagiza Mhandisi wa maji wilaya ya Kongwa kufika Mtanana haraka na kuanza kushughulikia kero hiyo ya maji ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji vizuri.

Sambamba na hayo nae mbunge wa Jimbo la Kongwa Mheshimiwa Joab Ndugai alisema kuwa wilaya ya Kongwa ndiyo iliyobeba dhamana kubwa ya ukombozi wa nchi za Afrika wakati zikipigania uhuru na sio sehemu nyingine kama watu wanavyoeleza.