Dodoma FM

Wakulima washauriwa kulima mazao ya muda mfupi

15 February 2022, 4:27 pm

Na; Neema Shirima.

Kutokana na kuwa na mvua za wastani katika mwaka huu wananchi wa mkoa wa Dodoma wameshauriwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili mvua za wastani

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa mtaa wa Pinda kata ya Zuzu jiji Dodoma Salvatory Laizer ambapo amesema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu kilimo cha mazao ya muda mfupi na yanayostahimili ukame kama vile alizeti na mihogo kutokana na mvua kuchelewa kunyesha

Amesema halmashauri ya Dodoma idara ya kilimo wamekuja na mpango mkakati wa kuuza mbegu kwa gharama nafuu ili wakulima waweze kumudu gharama hizo jambo ambalo limeleta hamasa kwa wakulima

Aidha kwa upande wa wakulima wamesema elimu ya kilimo cha mazao ya muda mfupi imewasaidia ila changamoto iliyopo ni wadudu wanaoshambulia mazao hayo ambapo wameiomba serikali iweke utaratibu wa kuwakopesha wakulima wadogo wadogo ili waweze kupata dawa ya kuulia wadudu hao

Jembe halimtupi mkulima ni maneno ambayo humtia moyo mkulima na wengi wao wanapofuata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo huwasaidia kupata mazao mengi na kumfanya afurahie shughuli za kilimo.