Dodoma FM

Wakazi wa Dodoma wametakiwa kutokuogopa kula mboga za majani

13 April 2021, 10:11 am

Na; Shani Nicolous.

Kufuatia kutoaminika kwa mboga za majani zinazouzwa  katika masoko yaliyopo jijini Dodoma wafanyabiashara wa mbogamboga wamezungumza na kutolea ufafanuzi juu ya ubora wa mboga hizo.

Wakizungumza na Dodoma fm wafanyabiashara hao wamesema kuwa mboga hizo zinalimwa sehemu safi na kumwagiliwa kwa maji ya kisima na hata zikiletwa sokoni huoshwa na kuwekwa sehemu safi kwaajili ya kuuzwa.

Wamesema kuwa wao pia  licha ya kuuza mboga hizo ni miongoni mwa watumiaji  na wanajali afya za walaji kwa kuzingatia usafi wa hali ya juu .

Aidha wamesema kuwa wanawaomba wateja wa mboga hizo wazingatie matumizi ya mboga za majani kwa wingi na waondoe hofu juu ya mboga za majani zinazo patikana sokoni kwani ni bora na zinafaa kwa matumizi.

Dodoma fm imezungumza na  Bw. Lazaro Milawi ambaye ni mkulima wa mbogamboga kutoka Ihumwa yeye anasema kuwa mboga hizo zinalimwa kwa kuzingatia  na kufuata njia zote  bora za kilimo na kujali afya za watumiaji.

Wataalamu wa afya wanashauri matumizi ya mboga za majani kwa wingi kwani mboga hizo zina kemikali rafiki kwa mwili kwa kuponyesha magonjwa na kuufanya uwe na kinga nzuri sana dhidi ya magonjwa mengi.