Dodoma FM

Wananchi watakiwa kujiunga na bima za Afya ili kujipatia matibabu kwa gharama nafuu

4 April 2022, 1:28 pm

Na;Victor Chigwada.

Serikali katika kuboresha huduma za afya imekuwa na mpango wa kutoa elimu na hamasa ya wananchi kujiunga na bima za afya zitakazo saidia kupatiwa matibabu kwa gharama nafuu

Hatahivyo pamoja na wananchi kuhamasika na bima za afya lakini mara kadhaa kumekuwepo na malalamiko juu bima hizo kwa kudai kutopata matibabu kama bima inavyojieleza

Moja ya wananchi wa kijiji cha Mita Kata ya Mvumi amesema kuwa wananchi wamekuwa wakipata usumbufu wa kupata matibabu ikiwa ni pamoja na kukosa dawa licha ya kuwa tayari wana bima za afya

Ameongeza kuwa ni vema Serikali kuboresha huduma ya afya kwa mfumo wa bima hususani bima ya CHF ambayo ipo chini ya usimamizi wa Wizara ya afya

Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Mita Bw.Alpha Zoya amesema kuwa hata hivyo kumekuwa na uduni wa huduma za afya katika kijiji chake kwani hawana zahanati wala Kituo cha afya hivyo wananchi kulazimika kutumia hospitali ya DCT ambayo ni gharama kumudu kwa watu wenye kipato cha chini

Naye Diwani wa Kata ya Mvumi Misheni Bw.Kenethi Chihute amekiri wananchi kupata changamoto upande wa afya kwani hospitali ya DCT iliyokuwa imeteuliwa kama hospitali ya Wilaya kwasasa imebaki na huduma binafsi baada ya ujenzi wa kituo cha afya Mlowa barabarani.

Pamoja na hamasa inayotolewa na Serikali kwa kushirikiana  na mashirika binafsi juu ya kila mwananchi kuwa na bima ya afya ni vyema Serikali kuendelea kuboresha namna ya upatikanaji wa huduma kiurahisi