Dodoma FM

Wazazi watakiwa kuhakikisha watoto wanaripoti shuleni Januari 8

6 January 2024, 4:07 pm

Picha ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mh. Rosemery Senyamule akiongea na wakazi wa Michese.Picha na Mkoa wa Dodoma.

Senyamule amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Michese unaotekelezwa katika kata ya Mkonze eneo la Michese na kuagiza kukamilika kwa ujenzi huo ili ifikapo tarehe 08 Januari wanafunzi waweze kukaa kwenye madarasa yenye ubora.

Na Seleman Kodima.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shuleni ifikapo tarehe 8 januari mwaka huu.

Ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Miradi ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Michese na kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Kata ya Mkonze eneo la Michese.

Picha ni Ukarabati wa Baadhi ya Majengo katika shule hiyo ukiwa unaendelea. Picha na Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza na wananchi wa Michese Mhe. Senyamule amesema mtoto atakaye chelewa kuanza Masomo kwa wakati atalima matuta kumi.

Sauti ya Mh. Rosemery Senyamule.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Justin Machela amesema tuwapeleke watoto wetu shule na kuepuka Malalamiko yasiyo na Msingi ili kuhakikisha watoto wanaanza masomo kwa wakati na kuwanunulia vifaa vinavyoitajika Shuleni kama madaftari na kalamu.

Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkonze Bw. Andrew Rumishaeli amesema shule ya Sekondari Mkonze ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 544 ikiwa ni fedha za Sequip kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 08 vya madarasa vyenye ofisi 02, Jengo la Utawala, Jengo la maktaba, Jengo la Tehama, vyoo vya wanafunzi matundu 08, Kichomea taka na Tanki la maji la ardhini.