Homa ya Ini inaweza kuingia mwilini bila kuonesha dalili
28 July 2026, 16:36

Ugonjwa huu unapo ingia mwilini huendelea kuharibu ini taratibu hadi kulisababisha kusinyaa na baadaye kupelekea saratani.
Na Jerome John.
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Homa ya Ini leo Jumanne, Julai 28, wataalamu wa afya wameonya kuwa ugonjwa huo unaweza kuingia mwilini bila kuonesha dalili zozote na kuendelea kwa miaka 10 hadi 20, ukiendelea kuharibu ini taratibu hadi kulisababisha kusinyaa na baadaye saratani.
Akizungumzia ugonjwa huo Daktari wa magonjwa ya ndani kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Swalehe Pazi amesema wagonjwa wengi wanaofika hospitalini huchelewa kutambua maambukizi hayo, hali inayopunguza nafasi ya matibabu yenye mafanikio na kuongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.
Virusi vya homa ya ini B huambukizwa kupitia damu na majimaji ya mwili yenye maambukizi, ikiwemo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua, kujamiiana bila kinga na mtu mwenye maambukizi, pamoja na kuongezewa damu isiyopimwa ipasavyo.