Dodoma kuimarisha usalama kwa kusimika kamera za ulinzi
2 June 2026, 16:43

kamera za ulinzi barabarani zitasaidia kudhibiti matukio ya uhalifu hali inayowapa wawekezaji uhakika zaidi wa mazingira salama.
Na Anwary Shaban.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026 umezindua mradi wa kusimika kamera za usalama wenye thamani ya shilingi 682,561,548.6, ukiwa na lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, mali zao pamoja na miundombinu ya umma.
Mradi huo umetekelezwa kwa ushirikiano ambapo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa kiasi cha shilingi 519,891,609.27, huku Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ukichangia shilingi 162,669,939.34 kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa ajili ya kuunganisha mfumo huo kupitia Mkongo wa Taifa.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Wazo Mwang’onda alisema ameridhishwa na mradi huo katika kuimarisha usalama wa Jiji la Dodoma na utasaidia kuvutia wawekezaji kutokana na mazingira salama yaliyopo.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Joseph Fungo alisema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 80, ukihusisha kusimika nguzo, kufunga kamera pamoja na vifaa katika chumba cha kuongozea.

Alieleza kuwa hatua zinazofuata ni kuunganisha kamera zote ili ziweze kusomana na chumba cha kuongozea kupitia Mkongo wa Taifa, kuingiza umeme wa gridi katika vituo 33 vya kamera, kutoa mafunzo kwa watumiaji, na kuandaa mfumo wa usimamizi katika kipindi cha matazamio.
Nae, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisema kuwa wamejifunza kutoka nchi mbalimbali na kubaini kuwa usalama ni nguzo muhimu katika miji ya kisasa.