Wajasiriamali Mpwapwa watakiwa kuzingatia kanuni za biashara
3 July 2026, 16:27

Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru WAPEDO Foundation kwa kuwawezesha. Wamesema elimu waliyoipata itawaongezea maarifa na kuwasogeza mbele kibiashara.
Na Stephen Noel .
Wajasiriamali Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, wametakiwa kuzingatia kanuni na taratibu za biashara ili waweze kukukuza mitaji yao na kufikisha biashara zao katika ngazi ya juu zaidi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mpwapwa, Bi. Fransica Mloka, wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku mbili kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la WAPEDO Foundation.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Bi. Mloka amesema ili wajasiriamali kufikia malengo ya kuwa na biashara kubwa na endelevu, ni lazima wazingatie kanuni muhimu za biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la WAPEDO Foundation, Mchungaji Anderson Madimilo, amesema pamoja na changamoto ya mitaji inayowakabili wajasiriamali wengi, upungufu wa elimu ya biashara umekuwa sababu nyingine kubwa ya wengi kupoteza mitaji yao.