Serikali yasisitiza umuhimu wa uimarishaji wa vipimo nchini
20 May 2026, 18:06

Kila Mwaka mei 20 Wakala wa Vipimo hushirikiana na Mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Vipimo Duniani kwa lengo la kuimarisha matumizi ya vipimo sahihi katika sekta mbalimbali za uchumi pamoja na maisha ya kila siku ya wananchi.
Na Mariam Kasawa.
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya vipimo nchini ili kuhakikisha vipimo vinakuwa sahihi, vinakubalika na kuaminika ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha sekta ya vipimo ili kulinda maslahi ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Amesema vipimo sahihi vina mchango mkubwa katika biashara, uzalishaji na maendeleo ya viwanda, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili vipimo vya Tanzania vitambulike na kuaminika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metrolojia (TBS) Bw. Ridhiwani Matange amesema maabara za vipimo zina jukumu muhimu katika kuhakikisha ubora wa bidhaa na huduma unazingatia viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.