Wagaga wa tiba asili wakumbushwa kuzingatia maadili wanapotoa huduma kwa wananchi
3 August 2026, 17:59

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya Sayansi Shirikishi Awamu ya Pili kwa mwaka 2026 wamesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwao kwani yamewaongezea uelewa wa kitaaluma, huku wakieleza kuwa sasa wanaweza kufanya kazi kwa kujiamini kutokana na kuwa na leseni pamoja na vyeti vya mafunzo.
Na Anwary Shabani.
Waganga wa tiba asili na tiba mbadala nchini wameaswa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya taaluma wanapotoa huduma kwa wananchi ili kujenga imani ya jamii, kuboresha huduma na kujiongezea kipato kupitia kazi zao.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya Sayansi Shirikishi Awamu ya Pili yaliyoandaliwa na Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (TAMESO-T) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Daktari Maira Biseko amesema waganga wa tiba asili wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za taaluma pamoja na kutunza siri za wagonjwa wao, jambo litakaloongeza heshima na imani ya jamii kwa huduma wanazozitoa.
Dkt. Biseko ameongeza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuendelea kujisomea na kupitia mara kwa mara mafunzo waliyoyapata ili kuongeza ujuzi na ubora wa huduma. Amesema hatua hiyo itasaidia kukuza sekta ya tiba asili nchini na kuiwezesha kutoa huduma zenye ushindani hata kwa wananchi kutoka nchi jirani ikiwemo Kenya na Uganda.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMESO-T Wilaya, Lucas Mlipu, ametoa shukrani kwa mgeni rasmi, wawezeshaji na washiriki wa mafunzo hayo kwa ushiriki wao mkubwa. Amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo waganga wa tiba asili kutoa huduma salama na zinazozingatia misingi ya taaluma.
Naye Diwani wa Kibaigwa, Daudi Kweka, amesema mafunzo hayo yatabadilisha namna wataalamu hao wanavyotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na ubora wa huduma. Amesisitiza kuwa huduma bora ndiyo njia sahihi ya kujitangaza, kwani mgonjwa anayepata matibabu mazuri ndiye atakayewaletea wagonjwa wengine.
Aidha, Mwenyekiti wa Mafunzo ya Wataalamu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Arusha, Dkt. Mussa Daudi, amewataka washiriki kuyatumia kwa vitendo maarifa waliyoyapata ili kuongeza ufanisi wa huduma wanazozitoa kwa jamii.