MOI yatumia akili unde kurahisisha huduma za matibabu
1 September 2026, 16:28

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za MOI kuhakikisha wananchi wanapata huduma za tiba za kisasa, salama na zenye ufanisi, huku matumizi ya teknolojia yakiendelea kuchukua nafasi muhimu katika sekta ya afya.
Na Anwary Shaban.
Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo muhimbili MOI imeeleza kuwa inaendelea kutumia teknolojia ya akili unde pamoja na mitambo ya kisasa kuboresha na kurahisisha huduma za matibabu hususani katika tiba ya mifupa na operesheni za ubongo .
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili, MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mipango ya taasisi hiyo katika Mwaka wa Fedha 2025/26.
Balozi Dkt. Ulisubisya amesema matumizi ya teknolojia hiyo yameenda sambamba na uwepo wa mitambo ya kisasa pamoja na wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kuitumia katika kuboresha huduma za afya.
Aidha, amesema tatizo la pingili za mgongo limekuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo, akieleza kuwa awali matibabu yalihitaji kufunguliwa sehemu kubwa ya mgongo, lakini kwa sasa teknolojia imewezesha kufanyika kwa njia rahisi zaidi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Ulisubisya amesema ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita, MOI imeanzisha huduma maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye viungo vilivyopooza kutokana na sababu mbalimbali, hatua inayolenga kuwapa nafuu na kuboresha maisha yao.