Kicheko, siri ya afya bora na kukabiliana na changamoto za maisha
27 August 2026, 16:36

Licha ya ugumu wa maisha, wataalamu na wanasaikolojia wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri, kupata muda wa kupumzika, kufanya mambo tunayoyapenda na kutafuta sababu za kucheka na kufurahia maisha.
Na Grace Budodi.
Kicheko ni sehemu ya maisha ya kila siku. Ni jambo dogo linaloweza kubadilisha hali ya mtu kwa muda mfupi—kutoka huzuni hadi furaha, kutoka ukimya hadi mazungumzo.
Wahenga wanasema, “Tabasamu ni nusu ya furaha.” Lakini je, kicheko kinaishia kwenye furaha pekee, au kinaweza pia kuwa na mchango katika afya ya mwili na akili?
Wapo wanaosema hawawezi kumaliza siku bila kucheka, Wanasema kucheka ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, na kwamba hata katikati ya changamoto, huwa wanatafuta sababu ya kutabasamu na kucheka.
Lakini nyuma ya vicheko hivyo, kuna jambo jingine linaloweza kuvutia zaidi, Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kitendo hiki tunachokifanya mara nyingi bila hata kukifikiria kinaweza kuwa na uhusiano na namna mwili na akili vinavyofanya kazi.
Na ndipo naamua kufunga safari hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Dodoma moja kwa moja nakutana na Dkt. Stephano Mwaisobwa, na anaeleza umuhimu wa kucheka na namna kitendo hiki kinavyoweza kuhusishwa na afya ya mwili.
Na si mwili pekee unaoweza kuguswa na kicheko. Akili na hisia nazo zina nafasi yake.
Katika maisha yenye changamoto, msongo na mawazo mbalimbali, kicheko kinaweza kuwa sehemu ya namna mwanadamu anavyokabiliana na hali yake ya kihisia.
Dkt. Chris Mauke yeye ni Mwanasaikolojia anaeleza umuhimu wa kucheka katika saikolojia ya mwanadamu.
Katika maisha yenye changamoto, furaha wakati mwingine huonekana kama kitu cha mbali. Gharama za maisha, majukumu ya kila siku, presha za kazi na changamoto mbalimbali zinaweza kumfanya mtu asahau hata la kutabasamu.
Lakini kama usemavyo msemo, “Maisha ni safari, si kituo.” Pamoja na ugumu unaoweza kujitokeza njiani, bado kuna nafasi ya kufurahia mambo madogo yanayotuzunguka.