TANROADS yaagiza ukaguzi wa miundombinu kukabiliana na mvua za el nino
8 September 2026, 16:36

Hatua hiyo ya TANROADS inakuja wakati mamlaka hiyo ikiweka mkazo katika maandalizi ya mapema ya miundombinu, kwa lengo la kupunguza madhara ya mvua na kuhakikisha usalama wa wasafiri pamoja na mwendelezo wa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Na Anwary Shabani.
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeziagiza Ofisi za Mameneja wa Mikoa yote 26 nchini kufanya ukaguzi wa haraka wa miundombinu ya barabara, madaraja, makalavati na maeneo mengine hatarishi, kwa lengo la kubaini changamoto na kuchukua hatua mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo, ambapo amesema ukaguzi huo ni muhimu kutokana na changamoto zinazojitokeza katika baadhi ya maeneo wakati wa mvua, ikiwemo kukatika kwa barabara na madaraja.
Mhandisi Besta ametolea mfano Daraja la Mutikila, ambalo Desemba mwaka jana liliathiriwa na mvua kubwa na kusababisha usafiri wa magari na wananchi kukwama, hali iliyosababisha usumbufu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Amesema maandalizi hayo ya mapema yanalenga kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, huku yakihakikisha usalama wa wasafiri na kuendelea kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.