Dodoma FM

WMA yawataka wananchi kuacha kununua kokoto na mchanga kwa ‘tripu’

19 September 2026, 12:37

Pichani Afisa Mtendaji Mkuu wa wakala wa vipimo (WMA), Alban Kihula alipokuwa katika Ofisi za Idara ya Habari – Maelezo akitoa maelekezo hayo. Picha na Anwary Shabani

WMA imewataka wananchi kutumia vipimo vinavyotambulika kisheria na kutoa taarifa pale wanapobaini ukiukwaji wa taratibu za vipimo, huku ikisisitiza kuwa matumizi ya vipimo sahihi ni muhimu katika kulinda haki za mnunuzi na muuzaji na kujenga biashara yenye uaminifu.

Na Anwar Shabani.

Wananchi wanaendelea kukumbushwa kuacha tabia ya kununua kokoto, mchanga na makaa ya mawe kwa kutumia idadi ya tripu za magari, badala yake kutumia kipimo rasmi cha ujazo kinachotambulika kisheria ili kuondoa migogoro na udanganyifu unaoweza kujitokeza katika biashara hizo.

Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihula, alipokuwa katika Ofisi za Idara ya Habari – Maelezo, ambapo amesema WMA inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa kwa vipimo sahihi na vinavyotambulika.

Kihula amesema wananchi wanapaswa kuangalia alama za ujazo zilizowekwa kwenye magari yaliyofanyiwa uhakiki na WMA, badala ya kutegemea idadi ya tripu wakati wa kununua kokoto, mchanga au makaa ya mawe.

Aidha, Kihula amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha, WMA imeendelea kuhakikisha mifumo ya vipimo katika mnyororo mzima wa upokeaji, usafirishaji na utoaji wa mafuta nchini inakidhi viwango vinavyotakiwa, hatua inayolenga kuhakikisha kiwango cha mafuta kinachopokelewa na kusafirishwa kinapimwa kwa usahihi.

Katika hatua nyingine, Kihula amesema WMA imefanya uhakiki wa jumla ya tanki 16,252 zinazotumika kusafirisha mafuta katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti upotevu wa bidhaa, tofauti za vipimo na migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wauzaji na wanunuzi.

Simulizi na Anwary Shabani.