Dodoma FM

Jamii yahimizwa kuipa kipaumbele lishe bora

24 August 2026, 17:30

Elimu kuhusu lishe bora inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi ili kuwajengea uelewa wa vyakula vinavyosaidia kujenga afya bora. Picha na Mtandao.

Baadhi ya wananchi wamesema bado kuna watu katika jamii ambao hawazingatii lishe bora licha ya elimu kutolewa mara kwa mara, hali inayowafanya kula kwa lengo la kukidhi njaa pekee bila kufahamu umuhimu wa mlo kamili katika kujenga afya na kusaidia kuzuia magonjwa.

Na Daniel Njau

Jamii, familia na watu binafsi wamehimizwa kuzingatia lishe bora kwa kula mlo kamili wenye virutubishi mbalimbali, ili kuimarisha kinga ya mwili, kulinda afya na kujikinga dhidi ya magonjwa.

Mtaalamu wa afya na lishe, Bi. Magreth Benjamini, amesema changamoto ya kipato kidogo ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wananchi kushindwa kumudu lishe bora, huku wengine wakishindwa kupata zaidi ya milo miwili kwa siku.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa namna vyakula vinavyoandaliwa na kuuzwa barabarani na katika maeneo mbalimbali pia inaweza kuchangia watu kutokuzingatia mahitaji sahihi ya lishe, kutokana na kula bila kuangalia ubora na virutubishi vinavyohitajika na mwili.

Kwa upande wake, mtaalamu wa afya kutoka kituo cha afya, Bwana George Kaishozi, amesema elimu kuhusu lishe bora inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi ili kuwajengea uelewa wa kuchagua na kutumia vyakula vinavyosaidia kujenga afya bora.

Sauti na Daniel Njau.