Dodoma FM

Taasis na mashirika yasiyo ya kiserikali yatakiwa kuzingatia sheria

26 June 2026, 13:01

Picha ni wakati wa akizindua rasmi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NaCoNGO.Picha na Anwary Shaban.

Muongozo huo unatarajiwa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi katika uendeshaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, sambamba na kuongeza mchango wao katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Na Anwary Shaban.

Serikali imezitaka Taasis na Mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kuzingatia sheria , uwajibikaji na ushirikiano kwa maendeleo ya Taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akizindua rasmi Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NaCoNGO ambapo amesema serikali imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma umewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii, viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na maafisa wa serikali, kwa lengo la kuimarisha utendaji na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.

 Dkt. Gwajima amesema amefarijika kuona kuwa muongozo huo mpya unasisitiza utamaduni wa kujipima kwa kutumia viashiria vya utendaji, kuimarisha utendaji wa kamati mbalimbali pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya taifa, hususan katika utoaji wa huduma za kijamii na kuongeza uelewa kwa wananchi katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NaCoNGO), Jasper Makala, amesema kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kufanya mapitio ya muongozo wa awali na kuandaa toleo jipya litakalokwenda sambamba na mahitaji ya sasa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Maswi, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yana nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 na kusaidia serikali kufikia malengo yake ya maendeleo.

Kwa upande wake, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, Vicknes Mayao, amewashukuru viongozi na wadau walioshiriki katika uzinduzi huo, akibainisha kuwa serikali imeendelea kuthamini na kutambua kazi zinazofanywa na mashirika hayo, huku akipongeza kuanzishwa kwa muongozo huo mpya.

Sauti ya Kina Anwary.