Dodoma FM

Wananchi watakiwa kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya watoto

2 July 2026, 16:37

Wananchi wametakiwa kutovumilia vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.Picha na Mtandao.

Kwa ujumla, wataalamu hao wameeleza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa kwa wakati, pamoja na kushirikiana na vyombo vya dola na watoa huduma za afya, ni hatua muhimu katika kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huku ukichangia upatikanaji wa haki kwa waathirika.

Na Mwandishi wetu.

Wananchi wamehimizwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto mara yanapotokea ili kuwezesha ukusanyaji wa ushahidi wa kisayansi kwa wakati, hatua inayosaidia kuimarisha uchunguzi na kuongeza uwezekano wa kupatikana kwa haki mahakamani.

Akizungumza na KM24 FM katika kipindi cha SANUKA, Muuguzi Salome Bujimu amesema ni muhimu mhanga wa ukatili hususani ubakaji asioge wala kufanya vitendo vinavyoweza kuharibu ushahidi kabla ya kufikishwa katika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

Ameeleza kuwa hatua hiyo husaidia kuhifadhi ushahidi wa kisayansi unaohitajika katika uchunguzi na uendeshaji wa kesi za ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Kwa upande wake, Afisa kutoka Dawati la Jinsia, Paskazia Pande, amesema ushahidi wa kisayansi una nafasi kubwa katika kuimarisha kesi mahakamani kwa kuwa hutoa vielelezo vinavyosaidia kuthibitisha tukio la ukatili na kuwawajibisha wahusika kwa mujibu wa sheria.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Magret Musa, amewataka wananchi kutovumilia vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, akisisitiza kuwa matukio hayo yaripotiwe ndani ya saa 72 tangu kutokea kwake ili kutoa nafasi ya ukusanyaji wa ushahidi muhimu wa kisayansi, pamoja na kuhakikisha waathirika wanapata huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na haki zao kwa mujibu wa sheria.

Sauti kina Leokadia.