Dodoma FM

TASAC na NBS zasaini makubaliano sensa ya vyombo vya usafiri

4 June 2026, 16:38

Picha ni hafla hiyo ya utiaji saini ambayo imefanyika katika Jengo la Takwimu jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka taasisi hizo mbili.Picha na Mtandao.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara ya mwaka 2026/2027 inatarajiwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kuboresha usimamizi, usalama na maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini nchini, huku ikiimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Na Anwary Shaban.

Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini Tanzania (TASAC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zimetia saini makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara ya mwaka 2026/2027.

Hafla hiyo imefanyika katika Jengo la Takwimu jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka taasisi hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ukusanyaji wa takwimu muhimu zitakazosaidia maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini nchini.

Akizungumza mara baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed  Malick ametoa shukrani kwa uongozi wa NBS kwa kukubali kushirikiana katika utekelezaji wa zoezi hilo la kitaifa, akisema ushirikiano huo utasaidia taifa kupata takwimu sahihi na za kuaminika kwa ajili ya kufanya maamuzi na mipango ya maendeleo.

Sauti ya Mohamed  Malick.

Amesema matokeo ya Sensa ya mwaka 2021 yalitoa taswira ya hali ya vyombo vya usafiri majini nchini na kuweka msingi wa kanzidata ya taifa ya vyombo hivyo, huku sensa hiyo ikisaidia kutambua maeneo yanayotoa huduma za usafiri majini pamoja na kukusanya takwimu muhimu za msingi.

Sauti ya Mohamed  Malick.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NBS Amina Msegwa amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza jukumu la uzalishaji wa takwimu rasmi kwa kuzingatia viwango na taratibu zote za kitaalamu, huku ushirikiano huo na TASAC ukiwa sehemu ya kuimarisha upatikanaji wa takwimu zitakazotumika katika tathmini na upangaji wa mikakati ya maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini.

Sauti ya Amina Msegwa

Ameongeza kuwa NBS imekamilisha maandalizi muhimu ya sensa hiyo kwa kuwajengea uwezo wataalamu, kuandaa dodoso pamoja na kuratibu hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hilo kabla ya kuanza rasmi.

Sauti ya Amina Msegwa

Naye Afisa wa TASAC, Nasoni Sigara, ameeleza kuwa makubaliano hayo yametokana na maridhiano ya pamoja kati ya taasisi hizo mbili kwa lengo la kuendeleza sekta ya usafiri wa majini, akibainisha kuwa sensa hiyo itachangia ukuaji wa sekta hiyo kupitia upatikanaji wa takwimu sahihi na za kisasa.