Dodoma FM
Dodoma FM
8 August 2025, 3:42 pm

Maadhimisho ya wakulima ya Nanenane mwaka huu yanafanyika kitaifa mkoani Dodoma, yakilenga kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Na Seleman Kodima.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya kilimo nchini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa weledi na bidii ili Tanzania iwe na akiba ya kutosha ya chakula ifikapo mwaka wa fedha 2029/30.
Akizungumza leo Ijumaa jijini Dodoma wakati wa ziara ya kukagua mabwawa katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kila kitengo katika mnyororo wa thamani wa kilimo kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

Rais Samia amesema kuwa sekta ya kilimo imeanza kuimarika na sasa ni wakati wa kuongeza kasi ya uzalishaji.
Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya kilimo ni msingi wa usalama wa chakula na ustawi wa taifa. Amehimiza matumizi ya teknolojia, utafiti wa kisayansi, na ushirikiano wa sekta binafsi na ya umma ili kufikia malengo ya taifa.