Dodoma FM

Wakazi wa Dodoma watakiwa kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu chanjo ya uviko 19

4 August 2021, 10:14 am

Na;Yussuph Hans.

Wakazi Mkoani Dodoma wametakiwa kuhakikisha watumia vyema fursa ya kupata chanjo ya Uviko-19 na kupuuzia taarifa za upotoshaji kutoka katika mitandao ya kijamii na za mtaani.

Wito huo umetolewa mapema leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh Antony Mtaka wakati wa uzinduzi wa chanjo ya UVIKO 19 ulioambata na zoezi la kuchanjwa kwa wakazi, viongozi wa dini na taasisi za serikali.

Mh Mtaka amesema ni vyema kutumia fursa hiyo kwa wakati, ambapo chanjo inapatikana katika vituo mbalimbali vya afya kabla ya kumalizika kwa zoezi hilo.

Kwa upande wake Mganga mkuu Mkoa Best Magoma, amesema kuwa katika awamu hii ya kwanza Dodoma imepata jumla ya chanjo 50,000 huku kadri chanjo itakavyopatikana itazidi kutolewa kwa wananchi.

Nao baadhi ya wabunge walioshiriki katika zoezi hilo akiwemo Mbunge wa Dodoma Mh Antony Mavunde na Mbunge wa Viti maalum Fatma Toufiq wameahidi kuendelea kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo dhidi ya mapambano ya virusi vya korona.

Zoezi la chanjo mkoani dodoma limeanza rasmi leo huku viongozi wakipata fursa ya kuchanjwa, huduma inayopatikana halmashauri zote katika vituo 28 vya afya.