Dodoma FM

Serikali yasisitiza umuhimu wa lishe bora shuleni

16 September 2022, 1:01 pm

Na; Alfred Bulahya.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema kuwa ili kupata matokeo mazuri ya elimu ni lazima kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora shuleni ili kuwajengea wanafunzi afya bora na kupata utulivu wa akili wawapo madarasani.

Akizungumza  Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya Utiaji Saini Fomu ya kujiunga na Muungano wa Chakula Shuleni Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh.Omary Kipanga amesema kuwa Pamoja na kuwepo kwa sera hiyo, utoaji wa huduma ya chakula shuleni umekuwa ukitekelezwa katika shule kwa namna na viwango tofauti.

Amesema Katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, upatikanaji wa matokeo mazuri ya elimu hutegemea afya aliyonayo mwanafunzi huku Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ikifafanua upatikanaji wa huduma muhimu katika shule na vyuo ikiwemo huduma ya chakula bora, maji safi na salama na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi.

.

Katika hatua nyingine ,amesema kuwa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni ni suala mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta na wadau mbalimbali na kwa upande wa Tanzania, Muungano huu, ni jukwaa muhimu la kupata uzoefu wa namna nzuri ya kutekeleza mpango wa chakula shuleni.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson amesema kuwa moja ya njia ya kufikia malengo kwa taifa lolote Duniani ni lazima kuwekeza kwa watoto hivyo ili kufikia huko lishe ni eneo linalohitaji maboresho makubwa.

.

Naye Mkuu wa Ofisi Ndogo ya Shirika la Mpango Chakula Duniani (WFP) Dodoma  Nima  Sitta amesema ni Muungano wa kimataifa wa chakula shuleni ni jukwaa la kuhakikisha nchi zote duniani ifikapo 2030 kila mtoto anapata angalau mlo mmoja shuleni.

Nao baadhi ya wanafunzi wakiwemo Beatrice Mtembi wa shule ya Sekondary Dodoma na  Lucas Mathias wa shule ya msingi ya Chifu Mazengo wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo muhimu kwani itasaidia kuongeza ufaulu darasani na kuepuka vishawishi vitakavyosababisha kutotimiza ndoto zao.