Umuhimu wa kuweka akiba ili kufikia malengo
16 June 2026, 17:38

Ni muhimu kutenga sehemu ya mapato mara tu yanapopatikana, kuandaa bajeti na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza uwezo wa kutimiza malengo yaliyowekwa.
Wananchi wametakiwa kujenga utamaduni wa kuweka akiba kama njia muhimu ya kufanikisha malengo yao ya maendeleo binafsi na familia, huku wengi wakikiri kuwa akiba imewasaidia kutimiza baadhi ya mipango waliyojiwekea katika kipindi hiki cha nusu mwaka wa 2026.
Baadhi ya wananchi waliozungumza wamesema mwanzoni mwa mwaka walijiwekea malengo mbalimbali ikiwemo kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kununua vifaa vya kazi na kugharamia elimu ya watoto.
Wananchi hao wamebainisha kuwa matumizi yasiyo ya lazima na ukosefu wa nidhamu ya kifedha ni miongoni mwa sababu zinazowafanya washindwe kufikia malengo yao kwa wakati. Wamesema watu wengi hupanga malengo makubwa mwanzoni mwa mwaka lakini hushindwa kuyafikia kutokana na kutotenga sehemu ya kipato chao kwa ajili ya akiba.
Kwa upande wake, mwanaharakati Bw. Asifiwe Shoni amesema akiba ni msingi wa mafanikio ya kifedha na kwamba mtu anapaswa kuanza kwa kuweka lengo analotaka kulifikia kabla ya kuamua kiasi cha kuweka pembeni.