Mpwapwa yatajwa kinara wa kusafirisha katoto kufanya kazi za ndani
5 August 2026, 14:24

Mamlaka zimewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kulinda haki za watoto kwa kuhakikisha wanapata elimu na malezi stahiki badala ya kuingizwa katika ajira za utotoni.
Na Stephen Noel.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Josephine Mwaipopo, ameonya vikali tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwatoa watoto wanaopaswa kuwa shuleni na kuwapeleka kufanya kazi za ndani, akisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria na haki za mtoto.
Akizungumza na Dodoma FM, Bi. Mwaipopo amesema kauli hiyo imefuatia tukio la mtoto kutoka Wilaya ya Mpwapwa ambaye picha yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii akiomba msaada wa kurejeshwa nyumbani baada ya kudaiwa kupelekwa kufanya kazi za ndani. Alisema baada ya juhudi za wadau mbalimbali, mtoto huyo alipatiwa msaada na kurejeshwa kwa familia yake katika Kijiji cha Bumila, Kata ya Lupeta, Wilaya ya Mpwapwa.
Bi. Mwaipopo alibainisha kuwa Wilaya ya Mpwapwa ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza katika Mkoa wa Dodoma kwa kusafirisha watoto kwenda kufanya kazi za ndani nje ya mkoa, hali ambayo imeendelea kuhatarisha ustawi na maendeleo ya watoto. Alisisitiza kuwa mamlaka zitaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Temeke, Bw. Ismail Sadiki, alisema bado kuna mabinti wawili wenye asili ya Mpwapwa waliopo Temeke ambao wanaendelea kufuatiliwa ili warejeshwe nyumbani kwao.
Naye mama mdogo wa mtoto aliyerejeshwa, Bi. Asha Leguna, amesema mtoto huyo hakuzoea mazingira ya mjini baada ya kufikishwa huko, hivyo alitoroka na kuonyesha nia ya kurejea kwa bibi yake aliyekuwa akiishi naye awali.