Wananchi wilayani mpwapwa walalamikia utupaji taka ovyo
18 September 2026, 16:50

Hali ya utupaji taka hovyo katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Mpwapwa imezua malalamiko miongoni mwa wakazi. Wakazi hao wanasema hali hiyo inachafua mazingira na kuhatarisha afya za wananchi. Wametaka mamlaka husika kuchukua hatua za kudhibiti tatizo hilo. Pia wamezitaka taka zinazokusanywa kusombwa kwa wakati ili kuzuia kurundikana.
Na Stephen Noel.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Mpwapwa wamelalamikia hali ya utupaji wa taka hovyo katika maeneo mbalimbali ya mji huo, wakisema hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wakazi na kuongeza hatari ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Wakizungumza na Dodoma FM, baadhi ya wakazi hao wamesema tatizo la taka limekuwa likijitokeza kwa muda mrefu bila kupata utekelezaji wa kutosha, hali ambayo, kwa mujibu wao, inachafua mazingira na kuufanya mji kupoteza mwonekano wake.
Aidha, wananchi hao wamezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kudhibiti utupaji wa taka hovyo, ikiwemo kuhakikisha taka zinazokusanywa katika maeneo mbalimbali zinasombwa kwa wakati ili kuzuia kurundikana.
Wamesema hatua hizo zitasaidia kuboresha usafi wa mazingira, kulinda afya za wananchi na kuufanya Mji wa Mpwapwa kuwa safi na wenye kuvutia.