Maendeleo ya teknolojia ya matibabu nchini yaongezeka
23 July 2026, 17:24

Kwa ujumla, uwekezaji huo katika teknolojia ya matibabu, miundombinu ya afya na rasilimali watu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya afya nchini, ili wananchi wapate huduma bora, za haraka na zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Na Anwary Shaban.
Serikali imesema kuwa maendeleo ya teknolojia ya matibabu nchini Tanzania yameongezeka kwa kiwango kikubwa, hatua inayochangia kuokoa maisha ya Watanzania kwa kuwapatia huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu.
Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akiwa jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya sekta ya afya na namna teknolojia mpya inavyorahisisha huduma kwa wananchi.
Msigwa amesema kuwa kwa sasa wagonjwa wanaweza kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia teknolojia maalum kwa kulala kwenye shuka, na majibu ya vipimo kupatikana kwa haraka, hatua inayorahisisha utambuzi wa magonjwa na kuanza matibabu mapema.
Ameongeza kuwa zaidi ya wananchi elfu ishirini na saba jijini Arusha tayari wamepatiwa huduma hiyo ya kisasa.
Aidha, Msigwa amesema Serikali imepeleka Shilingi Bilioni 9.75 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje pamoja na ununuzi wa mashine ya cathlab kwa huduma za moyo.
Amesema uwekezaji huo utasaidia kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bora za moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na kanda nzima ya nyanda za juu kusini.
Kwa upande mwingine, Msigwa amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kununua vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi hadhi ya kimataifa.
Ameeleza kuwa Serikali pia imeongeza idadi ya watumishi wa hospitali hiyo kutoka watumishi 20 mwaka 2015 hadi kufikia watumishi 1,076 kwa sasa, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.