Dodoma FM

Wakazi wa kata ya Mtanana wanatarajia kupitisha makubaliano ya kukodisha shamba lenye hekta 107

6 September 2021, 10:17 am

Na; Benard Filbert.

Ungozi wa kata ya Mtanana wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma unatarajia kupitisha makubaliano na wananchi ya kukodisha shamba lenye ukubwa wa heka 107 ili fedha hizo zitumike katika ujenzi wa madarasa pamoja na Zahanati.

Hayo yameelezwa na Diwani wa kata ya Mtanana bwana Joel Mussa wakati akizungumza na taswira ya habari ambapo amesema katika kuhakikisha wanaongeza madarasa katika shule ya msingi mtanana pamoja na nyumba ya mganga mkuu zahanati ya Mtanana B wameridhia kukodisha shamba lenye ukubwa wa heka 107.

Amesema shamba hilo litakodishwa kwa kipindi cha miaka 2 na fedha zitakazo patikana zitatumika kukamilisha ujenzi wa miundobinu ya majengo mbalimbali ikiwemo kituo cha polisi.

Kadhalika amesema kuwa wiki hii mnamo siku ya ijumaa kutakuwa na mkutano ili kutangaza rasmi kuhusu kukodishwa kwa shamba hilo.

Endapo shamba hilo lenye ukubwa wa heka 107 litakodishwa kwa kipindi cha miaka 2 itapatikana fedha kiasi cha milioni 10 ambazo zitasaidia ujenzi wa nyumba ya mganga katika zahanati ya Mtanana B madarasa 6 ya shule ya msingi mtanana pamoja na kituo kidogo cha polisi.