UWT Bahi walipongeza Dawati la Jinsia na Watoto
3 March 2023, 2:50 pm
Mkuu huyo ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za ukatili ili kumsaidia kila mmoja kuishi kwa furaha .
Na Bernad Magawa
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Dunuani ambayo hufanyika machi 8 kila mwaka, Jumuiya ya wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Bahi Wametebelea dawaji la jinsia na watoto Wilaya ya Bahi kujionea huduma zinavyotolewa.
Ziara hiyo iliyohusisha viongozi na Baadhi ya wanachama wa Jumuiya hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Bahi Imakulata Masigati imefanyika Machi 3,2023 kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika kimkoa wilaya ya Kondoa.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Imakulata ameeleza kufurahishwa na namna wanawake wilayani Bahi wanavyo hudumiwa katika kitengo hicho ambacho kinahusika na ukatili mbalimbali wa jinsia na watoto katika jamii huku akitoa rai kwa wananchi hususa ni wanawake kulitumia dawati hilo kutatua changamoto mbalimbali walizonazo.
“Nimefurahishwa na utendaji kazi wa Dawati, wanafanya kazi vizuri, ni wakarimu na wanasikiliza kwa makini bila ukali, hivi ndivyo huduma nyeti kama hii zinavyopaswa kutolewa kwa wananchi hasa wenye matatito kama haya ya unyanyasaji wa jinsia na watoto.” Amesema Masigati
Naye katibu wa Jumuiya hiyo Hilda Mdaki akizungumza katika ziara hiyo amewapongeza dawati la jinsia Wilaya ya Bahi kwa utendaji kazi mzuri na kueleza kuwa Watumishi wamekuwa wakiwahudumia wananchi kwa ukarimu mkubwa.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto wilaya ya Bahi Mkaguzi wa Polisi Edison Kaitaba amesema kwa kiasi kikubwa wanawake ndiyo wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupata huduma katika dawati hilo kuliko wanaume na kueleza changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa ni jamii kuficha taarifa za ukatili unaotokea katika jamii wanazoishi.
Mkuu huyo ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za ukatili ili kumsaidia kila mmoja kuishi kwa furaha na kusema kuwa unapotoa taarifa fiche kuhusiana na ukatili dawati lina utaratibu mzuri wa kumlinda mtoa taarifa asijulikane popote hivyo wananchi wasiogope kutoa ushirikiano kwa Polisi wa Dawati la Jinsia.